MWANANCHI
Aliyekuwa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu
aliyeamua kulitema taji hilo baada ya kubebeshwa kashfa amesema kuna
wakati alitaka kujiua lakini alirudisha moyo nyuma na kuona ingekuwa
shida kubwa nyumbani kwao.
“Sikuwa na
amani, niliishi maisha ya hofu, kujifungia ndani, kulia wakati wote.
Ilifikia hatua baba yangu alipata mshktuko kiasi cha kwenda kutibiwa
Afrika Kusini. Mama yangu pia alipata mshtuko…ningeweza kumpoteza.”—Sitti Mtemvu.
“Mama
yangu alisali na mimi, alinipigania, hakuonyesha hadharani jinsi gani
anaumia, lakini ukweli ni kwamba nilimwona alivyokuwa anadhoofu na
kukosa raha. Nyumba yetu iligeuka sehemu ya huzuni, amani ilitoweka ni
kama tulikuwa na msiba.”—Sitti Mtemvu.
Sitti anasema siku moja mama yake alimwambia kwamba aliumia siku alipompoteza mama yake lakini machungu aliyoyasikia kwa Sitti ni mazito zaidi japo baba yake wakati wote alivumilia na hakuonesha maumivu yake.
Anasema kuna wakati baba yake alikwenda
Afrika Kusini na akiwa huko alimtumia ujumbe wa kumuomba msamaha na
alimwambia kwamba hizo ni changamoto.
Sitti anasema alikuwa katika wakati mgumu kiasi cha kufikia uamuzi wa kutupa laini yake ya simu ya zamani.
MWANANCHI
Jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
limeibuka ghafla na kwa nguvu baada ya makada wa CCM kuanza kutangaza
nia, huku wengi wao wakionesha kuaminiwa na muasisi huyo wa Taifa na
wengine kuahidi kufuata miiko aliyoiweka wakati alipoongoza Serikali ya
Awamu ya Kwanza.
Makada wengine wametembelea kaburi la
Baba wa Taifa na wengine kutumia kuaminiwa kwake na wananchi wakati
akiwa na umri mdogo ili kujenga hoja kuwa uzoefu na umri si suala la
kuzingatiwa katika kupata kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwalimu Nyerere alikuwa na nguvu ya ushawishi na mkali dhidi ya rushwa na ufisadi jambo lililomfanya aheshimike ndani na nje ya nchi.
Miezi michache baada ya Bunge la Katiba
kuondoa mambo ya maadili kwenye Rasimu ya Katiba, suala hilo linaonekana
kurudi kwa nguvu kwenye sera za wagombea uongozi ambao wanataja kila
mara jina la Nyerere, miaka 16 baada ya kifo chake.
“Wanamtumia
Nyerere kwa sababu wanajua alikuwa muadilifu, alikuwa akisema kitu watu
wanatekeleza. Leo kiongozi anatoa maagizo hakuna anayetekeleza,” alisema mchungaji wa Kanisa la Pentekoste, Dk Damas Mukasa.
Mmoja wa Makada hao, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
alisema kuwa anatosha kushika wadhifa huo na kwamba Mwalimu Nyerere
atafurahi huko aliko iwapo atachaguliwa kuwa Rais kwa miaka 10 ijayo.
Membe alisema
kuwa Machi mwaka huu alikwenda Butiama na kuzuru kaburi la Mwalimu
Nyerere ambako alipiga magoti na kumweleza nia yake ya kuutaka urais.
Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Idara ya
Usalama wa Taifa, Dk Hassy Kitine naye alitumia jina hilo wakati
akitangaza nia ya kutaka kurejea Ikulu ambako alifanya kazi chini ya
utawala wa muasisi huyo, akiahidi kutumia miaka mitano kuirudisha
Tanzania ya Mwalimu Nyerere.
Dk Kitine alitumia sehemu kubwa ya
hotuba yake aliyoitoa mjini Dodoma kutoa mifano ya utendaji wa Mwalimu
Nyerere na kuwaponda wengine waliojitokeza kuwa hawana sifa za kumfikia.
HABARI LEO
Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha
INTEPOL wamefanikiwa kuwakamata watu 141 kwa makosa mbalimbali katika
Oparesheni iliyofanyika kwa siku mbili.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, CP Diwani Athumani
amesema baadhi ya makosa ambayo watu hao wamekamatwa yapo makosa ya
wizi wa magari, dawa za kulevya, silaha haramuna milipuko, wahamiaji
haramu na biashara haramu ya binadamu pamoja na wizi wa miundombinu ya
umeme na nyara za Serikali.
Katika magari 1,400 yaliyokaguliwa,
magari sita yaligundulika kuwa ya wizi na mengine matano yalichezewa
chesisi pamoja na pikipiki 12 nazo ziliibiwa.
Kati ya magari yaliyoibiwa, matatu yalitoka England, moja kutoka Hungary na jingine kutoka Tanzania.
HABARI LEO
Diwani wa Kata ya Kigamboni amesema wana
mpango wa kujenga uzio kuzunguka Shule mbalimbali zilizopo kwenye Kata
hiyo ili kukabiliana na tatizo la utoro wa Wanafunzi.
“Eneo la
Shule linatakiwa liwe salama ndio maana tunazijengea uzio, pia
kutapunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi na kuongeza ufanisi wa Shule
hizo”—Dotto Msawa, Diwani wa Kigamboni.
Diwani huyo amesema ujenzi huo utaanza
muda sio mrefu kwa kuwa tayari Mkandarasi amepatikana na kinachosubiriwa
ni kuypitishwa kwa Bajeti ya Serikali 2015/16.
NIPASHE
Waziri Stephen Wassira
ambaye pia ametangaza nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amesema yeye ndiye anayefaa kuwa rais wa nchi kwa sababu
anaichukia rushwa na hana kashfa yoyote.
Alisema nchi hii kwa sasa imejaa wala
rushwa na kwamba yeye ataikomesha kwa sababu anaichukia wala hajawahi
kuiomba au kuipokea, huku akisema kuwa kuna wanachama wenzake, ambao ni
wala rushwa wakubwa na kila kashfa wanaguswa lakini sasa wanataka
waingie Ikulu kwa kutumia rushwa waliyoivuna wakiwa madarakani.
Aidha, alisema akibahatika kuingia tano
bora na kisha tatu bora na badaye akapeperusha bendera ya CCM kama
mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama hicho, ni lazima viongozi wa
Ukawa watajinyonga kwa sababu wanamtambua jinsi alivyo na uwezo.
“Ukienda
hospitali utakutana na rushwa, polisi rushwa na mahakamani rushwa…
Rushwa imeanza zamani maana hata yule aliyekuwa akibeba mikoba ya Yesu,
lakini alivyopewa vipande 30 vya fedha akamsaliti Yesu, kwa hiyo rushwa
ni tatizo haikuanza leo, bali ya leo imezidi sana, ipo nyingine ya
mikataba mibovu, manunuzi, sasa akiwa Rais ambaye ni mla rushwa
atawaonea aibu wenzake.”—Waziri Wassira.
Alisema atahakikisha jembe la mkono kwa
wakulima linakuwa historia, ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa
vijana, kingine ni kuboresha elimu ya sayansi kwa wanafunzi wa
sekondari.
SOURCE: www.millardayo.com
0 Comments