NIPASHE
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, jana alichukua fomu ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema hakuupata wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), kwa kupewa kama zawadi au urafiki, isipokuwa alikidhi vigezo vya kiongozi aliyetakiwa kutoka Bara la Afrika.
“Ilikuwa ni zamu ya Afrika na
ilikuwa lazima atoke Tanzania, bahati ikawa kwa Asha-Rose, lakini si
kama inavyofikiriwa kwamba kuna urafiki, zawadi au hisani ilitolewa ndio
nikaipata. Uongozi katika UN unapitia mchujo, unachunguzwa kwa muda
mrefu na wala hakuna kupewa kazi kwa ujamaa,” Dk. Migiro.
Dk. Migiro alisema alichaguliwa kuwa
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutokana na uwezo wake pamoja na
sifa alizonazo; ndio maana Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-Moon, alimkubali pasipo shaka.
Waziri Migiro alisema uamuzi alioufanya
wa kutangaza nia ya kugombea urais, unatokana na CCM kupanua wigo wa
demokrasia kwa kuwawezesha wanachama wengi zaidi kujitokeza katika
mchakato wa kumtafuta kiongozi muhimu wa Taifa.
“Mazingira mazuri na mafanikio
yaliyojengwa na kufikiwa na CCM katika awamu zote nne, yamenisukuma mimi
kuwa mwanamke wa tatu kutangaza nia ya kugombea nafasi ya urais, kati
ya makada wengine 32 waliotangulia; nafarijika sana na wigo wa
demokrasia uliopo,” alisisitiza.
Kuhusu vipaumbele vyake akiteuliwa kuwa mgombea urais, Dk. Migiro alisema: “Nasubiri
ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoandaliwa ili niitumie kama
nyenzo kuu ambayo itakuwa imetaja maeneo yote muhimu.”
Hata hivyo, Waziri Migiro alisema
mafanikio yaliyofikiwa na serikali ya awamu ya nne, yamechochea ukuaji
wa uchumi na uboreshaji wa huduma za afya na hivyo kuongeza umri wa
kuishi kutoka miaka 45 hadi 60.
Dk. Migiro aliondoka nchini, Januari 5,
mwaka 2007 akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN na kuhudumu hadi
alipomaliza muda wake, mwezi Januari mwaka 2014.
Baada ya kurejea nchini, aliteuliwa kuwa
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), Idara
ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
NIPASHE
Ahadi zilizotolea na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 zinawatesa wabunge wengi wa CCM kutokana na baadhi kutokamilika.
Hali hiyo ilijitokeza jana bungeni katika kipindi cha maswali na
majibu, wakati wabunge wengi walihoji ni lini ahadi hizo zitakamilika.
Akiuliza swali la nyongeza, Mbunge wa Magu, Dk. Festus Limbu (CCM), alitaka kujua ni lini serikali itatekeleza ni mradi wa maji katika mji wa Magu.
Naye Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), alitaka kujua ni lini serikali itatimiza ahadi mbalimbali za ukamilishaji wa miradi ya maji katika jimbo hilo.
“Kuna ahadi nyingi ambazo zilitolewa na Rais Jakaya Kikwete,
lakini cha kushangaza miradi hiyo haijatekelezwa, sasa ni lini serikali
itakamilisha ahadi hizo” aliuliza na kuongeza:
“Naitaka serikali itoe kauli ni lini itatekeleza ahadi hizo ili
wananchi waondokane na adha ya maji ambayo inawafanya kushindwa kufanya
shughuli nyingine za maendeleo.”
Akijibu, Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, alisema ahadi zote zilizotolewa na rais zitatekelezwa.
Hata hivyo, alisema tatizo kubwa ambalo linasababisha baadhi ya miradi kutokutekelezeka kwa wakati ni ufinyu wa bajeti.
Alisema serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha miradi mbalimbali
ya maendeleo inakamiliswa ukosefu wa fedha za kutosha imebaki kuwa
changamoto kubwa.
HABARILEO
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wassira
amesema yupo tayari kumuunga mkono mgombea yeyote atakayeteuliwa na CCM
kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu, endapo nafasi
hiyo haitaangukia mikononi mwake.
Pamoja na ahadi hiyo, amesema hawezi
kutoa jibu lolote kwa sasa kama atagombea tena au hatagombea ubunge
katika jimbo lake la Bunda kwani haijaingia katika kinyang’anyiro hicho
cha urais kwa ajili ya kushindwa.
Akizungumza na wanahabari kabla ya
kukutana na wadhamini wake zaidi ya 100 waliojitokeza kumdhamini mjini
Iringa jana, Wassira alisema; “mimi ni mtu mwenye uzoefu mkubwa wa kuongoza Watanzania, kwa hiyo ninaamini nina fursa kubwa zaidi ya kuwa mgombea.”
Alisema hashangazwi hata kidogo kwani
CCM ina hazina ya viongozi wengi wenye sifa za urais japokuwa katika hao
waliojitokeza hakuna anayemhofia.
“Tofauti na wale wenzetu, wao wana
mtu mmoja mmoja tu katika vyama vyao, ukizungumza CUF utamtaja Lipumba
(Ibrahim) na vyama vingine ni vivyo hivyo; ni sasa tu baada ya
kuunganisha vyama vyao kupitia umoja usio rasmi angalau unaweza kuona
kama wako wengi, lakini kiuhalisia ni wale wale wanaotegemewa na vyama
vyao,”alisema.
HABARILEO
Wakati mwili wa Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Issa Bin Shaaban Simba aliyefariki dunia jana asubuhi ukitarajiwa kuzikwa leo jioni mkoani Shinyanga, Rais Jakaya Kikweteameungana na Waislamu wote nchini na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)kuomboleza kifo cha kiongozi huyo wa juu wa kiroho nchini.
Kwa mujibu wa habari kutoka ndani ya
familia, Mufti aliyefikwa na mauti akiwa katika Hospitali ya TMJ, Dar es
Salaam alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa sukari
na shinikizo la damu, atazikwa leo kutokana na wosia aliokuwa ameuacha
kuwa, akiaga dunia mwili wake usiachwe muda mrefu bila kuzikwa.
Hata hivyo, taarifa kutoka Bakwata
zinasema kwa upande wao wanatarajiwa kuuhifadhi mwili wa Mufti kesho au
keshokutwa, kwani alikuwa mtu wa watu hivyo kuna umuhimu wa kutoa fursa
kwa wengi kutoa salamu zao za mwisho kwa mpendwa wao.
Mmoja wa watoto wa marehemu, Selemani Simba alisema mwili utasafirishwa kwa ndege leo saa 3:00 asubuhi kuelekea mkoani Shinyanga, ambako atazikwa katika eneo la Majengo.
“Hali yake ilibadilika siku ya
Ijumaa ambapo tulimkimbiza Hospitali ya TMJ ambako baada ya kufanyiwa
vipimo ikabainika mapafu yalikuwa yamejaa maji hivyo ilitakiwa afanyiwe
upasuaji,” alisema.
Alisema baada ya kufanyiwa upasuaji huo
juzi, madaktari waliagiza mgonjwa apewe muda wa kupumzika na
asisumbuliwe, hivyo hakuweza kuzungumza na mtu yeyote hadi umauti
ulipomfika jana saa 3:45 asubuhi.
Rais Kikwete Katika salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete alisema; “Kifo
kinaleta huzuni, hata hivyo kifo hakizuiliki, hatuna budi kukikubali na
ni wajibu wetu kumuombea Shehe Mkuu kwa Mola wetu ampe mapumziko ya
milele”.
“Nawaombea subra wana familia, ndugu, jamaa, Waislamu wote na wana jamii kwani Mufti alikuwa kiongozi katika jamii yetu,” Rais alisema na kueleza kuwa, “Kamwe mchango wake hautasahaulika katika jamii yote kwa ujumla na hakika sote tutamkumbuka.”
Mufti Simba alijiunga na BAKWATA mwaka
1968 na amekuwa mwalimu wa chuo katika mikoa mbalimbali ya Mwanza,
Bukoba na mwaka 1970 alikuwa Shehe wa Mkoa wa Shinyanga.
Rais alimwelezea Mufti kama mwalimu
katika jamii ambaye alikuwa na uzoefu wa hali ya juu na mwenye kupenda
dini yake na kuitumia kwa manufaa ya jamii iliyomzunguka.
“Amekuwa mwalimu imara na mtu wa kutumainiwa na kutegemewa katika Uislamu na jamii kwa ujumla, hakika tutamkumbuka siku zote.”
MWANANCHI
Kambi rasmi ya upinzani bungeni imesema Serikali inatakiwa kukusanya
Sh19.6 trilioni kwa mwaka tofauti na malengo iliyojiwekea ya Sh13.4
trilioni, huku ikihoji sababu za miradi ya maendeleo kutegemea mikopo
ambayo alisema imeongeza ukubwa wa deni kwa wananchi.
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti Mbadala jana, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatiaalisema lengo hilo linaweza kufikiwa endepo Serikali itaweka mazingira mazuri na rafiki kwa mlipakodi.
Mbatia, aliyeingia kwa staili ya aina yake akionyesha mkoba uliobeba bajeti, alisindikizwa na Mchungaji Peter Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, Moses Machali (Kigoma Kasulu), Salum Barwani (Lindi Mjini) na Mustapha Akonay (Mbulu).
Mbatia alitaja njia nyingine za kuongeza mapato kuwa ni kupunguza
misamaha ya kodi isiyokuwa na tija hadi kufikia asilimia moja ya Pato la
Taifa, kuongeza ufanisi Bandari ya Dar es Salaam na kuweka mazingira
mazuri na endelevu katika sekta ya utalii.
Mbatia alirejea wito wa kila mwaka wa wapinzani wa kutaka juhudi
zaidi kuwekwa katika kupanua wigo wa vyanzo vya mapato katika sekta kama
uvuvi, maliasili, nyumba na ardhi.
Alisema Serikali ipanue wigo wa kodi, kuweka sera na viwango vya kodi
vinavyotabirika na endelevu, kuongeza ufanisi wa TRA kwa asilimia 50 na
kudhibiti ukwepaji wa kodi.
“Tutaweza kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi hadi kufikia
asilimia 20 mpaka 25. Washindani wetu wakubwa katika ukanda huu wa
Afrika Mashariki wanakusanya mapato kwa asilimia 22 ya Pato la Taifa, na
hawana mazingira mazuri ya uwekezaji na rasilimali nyingi kama
Tanzania,” Mbatia.
Mbatia aliendelea kubainisha sura ya bajeti mbadala kuwa mapato ya
kodi na yasiyo ya kodi yatakuwa ni Sh18 trilioni na mapato ya
halmashauri kuwa Sh848.1 bilioni.
Alisema mikopo na misaada ya kibajeti ni Sh660 bilioni huku mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo ikiwa ni Sh1.6 trilioni.
Alisema mikopo na misaada ya kibajeti ni Sh660 bilioni huku mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo ikiwa ni Sh1.6 trilioni.
Msemaji huyo wa Kambi ya Upinzani alilinganisha bajeti ya Serikali na
bajeti mbadala na kusema bajeti mbadala haina mikopo ya kibiashara,
hivyo inalenga kulipunguzia taifa mzigo wa madeni.
“Bajeti ya Serikali ina mikopo ya kibiashara ya asilimia 10, bajeti hii inawaongezea wananchi mzigo wa madeni,” alisema Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Alisema hivi sasa kila Mtanzania anadaiwa Sh873,904.56 kutokana na deni la Taifa kuzidi kukua.
MWANANCHI
Watu 23 wamekufa papo hapo na wengine 34 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni yaAnother G
kugongana na lori eneo la Kinyanambo A, Mafinga wilayani Mufindi, ikiwa
ni takriban miezi mitatu baada ya ajali nyingine iliyoua watu 50 katika
wilaya hiyo.
Basi hilo, lifanyalo safari zake kati ya Iringa na Njombe, lilipata
ajali hiyo saa 1:45 usiku wa kuamkia jana wakati dereva alipokuwa
akijaribu kuyapita magari mengine kabla ya kugongana uso kwa uso na
lori.
Kaimu kamanda wa polisi wa Mkoa wa Iringa, Pudenciana Protas alisema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Nicholaus Mangula na lori la Kampuni ya Bravo Logisticslililokuwa likiendeshwa na Rogers Mdoe na ambalo lililikuwa likitokea Zambia kuelekea Dar es Salaam.
Katika ajali hiyo, dereva wa lori alifariki dunia papo hapo.
Machi 10 mwaka huu, watu 50 walipoteza maisha kwenye ajali iliyotokea
Mafinga, Changarawe, wakati kontena lililokuwa limebwa na lori
lilipochomoka wakati dereva akijaribu kukwepa mashimo barabarani na
kuangukia kwenye lori.
Alisema majeruhi wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi mjini
Mafinga na maiti zimehifadhiwa hospitalini hapo ikiwamo ya dereva wa
lori aliyekufa papo hapo.
Alisema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi la Kampuni ya
Another G ambaye alikuwa kwenye mwendo kasi na alikuwa akiyapita magari
mengine bila tahadhari ndipo alipofika katikati alikutana na lori na
kuamua kulichepusha nje ya barabara hali iliyosababisha kupinduka na
kisha lori kuligonga basi hilo ubavuni.
Alisema baada ya ajali hiyo, dereva wa basi alikimbia lakini polisi wamemkamata na yupo chini ya ulinzi.
MTANZANIA
Hekaheka za kusaka wadhamini mikoani kwa
makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaowania kugombea urais
zimeendelea kushika kasi mikoani.
Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti Mstaafu na kada mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera, Pius Ngeze ametangaza rasmi kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika harakati zake za kutafuta kuwa mgombea urais kupitia chama hicho.
Ngeze aliyekuwa miongozi mwa viongozi wa
chama hicho mkoani humo waliojumuika katika mapokezi ya Lowassa
aliyewasili mjini Bukoba saa 6.00 mchana akitokea Sumbawanga, alisema
kama alivyomuunga mkono Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 na akashinda, pia
anamuunga mkono Lowassa.
“Leo ndiyo leo. Kila siku
mnaniuliza, Mzee Ngeze uko wapi… Sasa leo nawatangazia rasmi mbele yenu.
Kama nilivyomuunga mkono Rais Kikwete mwaka 2005 na akashinda,
natangaza Kagera na dunia nzima, namuunga mkono Lowassa… hata kwenye
fomu ya udhamini nimekuwa mtu wa kwanza,” alisema Ngeze huku akishangiliwa na umati wa wanachama na wapenzi wa CCM katika ofisi ya chama hicho mkoa.
Akitaja sababu ya kumuunga mkono Lowassa, Ngeze alisema haoni mgombea mwingine wa kumshinda na kwamba ana uamuzi mgumu.
“Ukiangalia wagombea wote walio
nyuma yake, yeye ndiye kiongozi pekee anayeweza kuingia Ikulu na
kudumisha yale yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete.
“Anajulikana kwa uamuzi mgumu na
nchi yetu inahitaji watu wenye uamuzi kama huo. Lowassa hajawahi
kuajiriwa na Serikali, tangu alipomaliza chuo kikuu alichukuliwa pamoja
na Rais Kikwete na wengine wawili kukitumikia Chama cha Mapinduzi,” Ngeze.
Aliendelea kumwagia sifa Lowassa akisema
ndiye aliyejenga shule za sekondari za kata na kuvuta maji kutoka Ziwa
Victoria kwenda mikoa ya Shinyanga na Tabora.
Lowassa akiwashukuru wana CCM
waliomdhamini kuwania kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM, alisema
kupata wadhamini wengi ni kufunga bao la urais.
“Nawashukuru sana kwa mapokezi
makubwa mliyonipa. Wadhamini wanaotakiwa kila mkoa ni 30 tu, lakini
nikipata 2000, 4000 au 7000 nashukuru kwani inaonyesha imani na upendo
wenu kwangu. Imani hujenga imani… Niliwaambia Shinyanga kuwa ukiona watu
wengi ujue umefunga bao na ninyi ndiyo mtaniwezesha kufunga,” Lowassa.
Akizungumzia sababu ya kugombea urais,
Lowassa alisisitiza kuwa anachukia umasikini hivyo anataka kupambana nao
kwa mwendo wa mchakamchaka.
“Nakerwa sana na umasikini. wapo
baadhi ya viongozi wanaovaa nguo mbaya wanadhani ni sifa. Ni aibu kuwa
masikini, ni aibu kuishi chini ya dola moja kwa siku, nikishinda
nitapambana na umasikini kwa mwendo wa mchakamchaka”, Lowasssa.
Alisema ili kufikia maendeleo ya kweli ni lazima kubadilishwa mtazamo wa kazi na watu wafanye kazi kwa bidii.
0 Comments