Habari

6/recent/ticker-posts

Header Ads Widget

Advertise with us here

MAGAZETINI LEO || NEWS PAPERS - TZ


MWANANCHI
CCM imesema kuwa itahakikisha inarudi Ikulu hata “kwa bao la mkono” wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya Nyehunge wilayani hapa.
Neno “bao la mkono” hutumiwa kama goli lililofungwa kwa kuupiga mpira kwa mkono kinyume cha taratibu za mpira, lakini hukubaliwa kwa kuwa mwamuzi anakuwa hajaona kitendo hicho.

“Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono… bao ni bao tu ili mradi refa hajaona,”Nape.

Nape, aliye kwenye ziara ya katibu mkuu wa CCM, aliwataka wananchi wa Sengerema kusubiri ushindi wa chama hicho na kuwakumbusha kuwa wanapaswa kuiweka CCM kuanzia udiwani mpaka ubunge kwa nafasi ya urais tayari kuna uhakika.
Katika mkutano huo, Nape alisema ana uhakika CCM itashinda baada ya kushuhudia mwitikio wa Watanzania tangu alipoanza kuongozana na Kinana katika ziara zake za kuizunguka nchi na kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero zao.
Amebainisha kuwa amejifunza na kujiridhisha kuwa chama chake bado kinapendwa miongoni mwa wapigakura waliofikiwa tofauti na vyama vya upinzani.


“Tumefika maeneo mengi ambayo upinzani haujafika. Huko tuna hazina kubwa ya wanachama. Hakuna namna Ukawa wanaweza kuingia Ikulu mwaka huu,” alisisitiza.

Kauli hiyo ya Nape ilipingwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani waliosema kuwa mtendaji huyo anamaanisha kuwa CCM itaiba kura.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa hakutaka kabisa kuzungumzia kauli ya Nape zaidi ya kusema watakutana Oktoba.

“Kwa bahati mbaya kauli za Nape siwezi kuzijibu. Kauli za Nape zichukue kama zilivyo, ingekuwa ni (katibu mkuu wa CCM, Abdulraham) Kinana, ningemjibu lakini ajue kuwa tutakutana Oktoba,” alisema Dk Slaa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo.

MWANANCHI
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limemtangaza Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally kukaimu nafasi ya mufti na sheikh mkuu.
Uteuzi huo unatokana na kifo cha Mufti Issa Shaaban Bin Simba siku saba zilizopita.
Katibu mkuu wa Bakwata, Suleiman Lolila alisema uchaguzi wa kumpata kaimu mufti ulifanywa kwa siku saba tangu kufariki kwa Mufti Simba.
Mufti Simba alifariki dunia Juni 15, mwaka huu katika hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na kisukari na alizikwa mkoani Shinyanga.
Lolila alisema waliomchagua Kaimu Mufti Ally ni wajumbe wanane wa Baraza la Ulamaa ambao walikutana na kupiga kura na kwamba Sheikh Ally alipata kura zote nane.

“Tulikuwa tunahangaika kwa siku saba kumtafuta kaimu mufti na hatimaye tumempata leo asubuhi. Atakuwapo madarakani kwa siku 90 hadi atakapochaguliwa Mufti,”  Lolila.

Kaimu Mufti Ally alisema atahakikisha Bakwata inaitisha uchaguzi wa mufti katika muda uliopangwa kikatiba.

“Kwa mujibu wa Bakwata nafasi ya kaimu mufti inakaimiwa kwa siku 90, hivyo nitashirikiana na viongozi wenzangu kuhakikisha tunaratibu na kufikia mkutano mkuu wa kumchagua mufti mkuu, Mufti Ally.

Alisema Bakwata itashirikiana na Baraza la Ulamaa kuhakikisha wanaweka umoja ndani na nje ya Uislamu na ataendeleza yote ambayo yalifanywa na mtangulizi wake katika kuendeleza imani na kupunguza migogoro baina ya jamii moja na nyingine.
Alisema atahakikisha wanafanya mabadiliko ya katiba ya Bakwata ili kuondoa matatizo yaliyopo sasa kwenye chombo hicho na baina ya Waislamu.
Alisema matarajio yake mengine ni kuendeleza yote mazuri aliyoyaacha marehemu Mufti Simba, hivyo ataunganisha mapya ya kujenga Uislamu.
Kaimu Mufti Ally alisema atashirikiana na viongozi wenzake wa safu ya utendaji kwa ajili ya kuiboresha Bakwata na atakuwa tayari kupokea ushauri.

MWANANCHI
Rais wa Simba, Evans Aveva alitumia dakika 17 kutangaza mabadiliko ya benchi la ufundi la timu hiyo litakalokuwa chini ya kocha Muingereza Dylan Kerr.
Kerr ambaye ni beki wa zamani mwenye miaka 48, alikuwa na mafanikio makubwa kama mchezaji kabla ya kugeukia ukocha.
Katika miaka tisa ya uchezaji soka, Kerr amecheza Ligi Kuu England akiwa na klabu za Leeds United na Reading FC, pamoja na Arcadia Shepherds FC ya Afrika Kusini mwishoni mwa miaka1980.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kocha Kerr ataigharimu Simba kiasi cha dola 9,000 ( Sh20 milioni) kila mwezi, kwani katika fedha hizo kocha huyo atakuwa akipokea kiasi cha dola 6,000 (Sh 13.2milioni ) kwa mwezi huku kiasi kinachobaki kitatumika kumlipia gharama mbalimbali za nyumba na usafiri.
Akitangaza mabadiliko hayo, Aveva alisema kocha Kerr atawasili nchini mwishoni mwa wiki tayari kuchukua nafasi ya Mserbia Goran Kopunovic.
Aveva alisema Kerr atasaini mkataba wa mwaka mmoja, pia kutakuwa na uwezekano wa kuongezewa mwingine endapo atafanya vizuri licha ya kuwa hana uzoefu wa kufundisha soka Afrika Mashariki, lakini amewahi kufanya kazi nchini Afrika Kusini.

“Tulikuwa na makocha kama watano ambao tulikuwa tunawaangalia katika kumpata mmoja, hata huyo Kim (Poulsen) alikuwapo ingawa siyo kama ambavyo inatamkwa ila baadaye tukaamua tumpe nafasi Kerr,” Aveva.

“Tunaamini Kerr ataisaidia Simba kupata mabadiliko makubwa katika Ligi Kuu, kazi yetu kama uongozi ni kumuandalia mazingira mazuri ya kufanya kazi akiwa na wasaidizi wake,”.

Kerr kabla ya kutua Simba aliwahi kufundisha klabu ya Hai Phong ya Vietnam pamoja na Mpumalanga Black Aces ya Afrika Kusini huku akitumia muda mwingi kuwa kocha msaidizi katika klabu mbalimbali.
Kerr atakuwa akisaidiwa na Seleman Matola pamoja na kocha mpya wa makipa Mkenya Abdul Idd Salim.

NIPASHE
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, amesema tuhuma alizotoa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) kuwa jeshi lake linamwonea kwa kumkamata na kumuweka mahabusu ovyo, wakati yeye sio mhalifu siyo za kweli na kwamba Mbunge huyo amekuwa chanzo cha vurugu katika uandikishwaji wa daftari la wapigakura.
Sabas alisema jana kuwa  Lema anasababisha vurugu kwa kutembelea maeneo ambayo watu wamejitokeza na kujiandikisha na kuhutubia, kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

“Yeye kama anataka kuhamasisha watu hatukatai, aende maeneo ambayo daftari bado halijafika akahamasishe na likifika aache wananchi wajiandikishe na siyo kuwafuata kwenye mistari na kuanza kupiga hatuba, siyo sahihi,” alisema.
Aliongeza: “Kwanini anapokuwapo Lema vurugu zinatokea, asipokuwapo hakuna vurugu, yeye asiende kwa watu ambao tayari wamejitokeza kujiandikisha, aende kwa ambao bado hawajafikiwa na daftari hilo.”

Sabas alisema kuwa Jeshi la polisi haliwezi kuonea mtu wala yeye (Lema) isipokuwa likipata taarifa kama siku ya tukio ya Juni 20 alipokamatwa kuwa analeta vurugu na wananchi hawataki kumwona katika maeneo ya uandikishaji ndipo walipokwenda kumkamata.
Alisema siku ya tukio walipata taarifa kutoka kwa askari walioko doria kwenye kituo cha Olsunyai kuwa kuna vurugu zinazofanywa ma Mbunge huyo na kuomba ulinzi uongezwe na askari wakapelekwa zaidi na kumtia mbaroni na wenzake 24 na aliyetoa taarifa polisi aliomba ulinzi.

“Lakini pia Lema anaongozana na kundi la watu toka maeneo tofauti ya uandikishaji, kitu ambacho siyo sahihi pia nacho kinakera baadhi ya watu,” alisema.

Hata hivyo, alisema uchunguzi dhidi ya tuhuma zake unaendelea na ukikamilika atachukuliwa hatua stahiki.

NIPASHE
Uandikishaji wa Daftari la Wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) katika maeneo ya wilaya ya Magharibi A, Zanzibar jana ulianza kwa dosari na kusababisha vurugu katika baadhi ya vituo.
Vurugu hizo zilitokana na sababu mbalimbali ikiwamo uchache wa vifaa vya uandikishaji na hamasa kubwa ya wananchi kutaka kujiandikisha.
Katika uandikishaji huo unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ni kuandikisha wapigakura ambao wana sifa za kuandikishwa ikiwamo umri wa miaka 18 kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Kutokana na vurugu hizo ikiwamo watu kupigana na kusukumana ili kupata fursa ya kujiandikisha, askari polisi na vikosi vingine vya ulinzi walimwagwa katika vituo mbalimbali ili kudhibiti uwezekano wa kupotea kwa amani.
Vurugu hizo pamoja na mambo mengine, zilisababishwa na wingi wa watu waliojitokeza na kusababisha changamoto kubwa kwa waandikishaji.
Baadhi ya vituo vilivyokumbwa na vurugu hizo ni Mtoni na Mtoni Kidatu katika wilaya hiyo huku wananchi wakilalamikia uchache wa BVR.

“Tupo hapa toka saa kumi na mbili asubuhi, lakini zoezi haliendi vizuri, tatizo lililopo ni uchache wa mashine, mashine moja tu ndio inayotumika na kama hali unavyoiona watu ni wengi sana,” alisema Asha Makame Haji katika kituo cha Mtoni.

Aidha, alisema idadi kubwa ya watu waliofika kujiandikisha ilitokana na baadhi yao kutokuwa wakazi wa eneo husika
Msimamizi wa kituo cha uandikishaji cha Kibweni,  Omar Ali Khamis, alisema uandikishaji unaendelea vizuri na wananchi hasa vijana wamehamasika kufika kujiandikisha, lakini changamoto zilizopo katika kituo hicho ni baadhi ya wananchi kuchanganya vituo vyao vya kujiandikisha na kwenda katika vituo ambavyo sio vinavyowahusu.
Afisa mmoja kutoka ZEC ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema mashine za BVR walizonazo zinatosheleza kwani uandikishaji katika kila wilaya utachukua siku nne na watu wote wataandikishwa na hakuna atakayenyimwa haki yake.
“Zoezi linaenda vizuri isipokuwa wananchi wana haraka, wanataka lazima wote waandikishwe siku moja wakati bado siku zipo za uandikishaji,”

HABARILEO
Idadi ya wagombea wanaochukua fomu kwa ajili ya kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana walifikia 39 baada ya mwanachama wake, Ritha Ngowi kuchukua fomu.
Ngowi, mkazi wa Dar es Salaam, anakuwa mwanamke wa tano kuchukua fomu, ambapo waliochukua fomu wa awali ni Balozi Amina Salum Ally, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Asha-Rose Migiro, Dk Mwele Malecela na Monica Mbega.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema yeye ni msomi ambaye ana shahada ya Maendeleo ya Jamii na pia amepitia kozi mbalimbali katika ngazi za diploma na cheti.
Alisema vipaumbele vyake vitakuwa ni kwenye sekta ya elimu na uchumi.

“Nimeguswa sana na kuamua kugombea nafasi ya Urais lengo langu kubwa ni kutaka kuboresha elimu na Uchumi” alisema.

Alisema iwapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha kila Mtanzania anapata elimu ya msingi na asiwepo Mtanzania asiye na uwezo wa kupata kipato na atahakikisha Watanzania wanawezeshwa ili kuwe na uzalishaji.
Kwa upande wa uchumi alisema atamairisha vivuko kwa ajili ya kupunguza foleni, na wakulima watapatiwa pembejeo na mazao yao yatatafutiwa masoko.
Hata wafanyabiashara kazi zao katika mazingira mazuri na wafanyakazi wa serikali watapata mishahara mizuri itakayowezesha wananchi kuishi maisha yenye viwango. Alisema atarekebisha mishahara kuanzia ngazi ya chini.

“Unaweza kuona mtu anapokea mshahara wa Sh 350,000 hadi 450,000 anapanga nyumba na analipa ada, maslahi yao lazima yarekebishwe,” alisema.

Alipohojiwa kama ana sifa 13 za mgombea wa CCM anavyo alisema anazo sifa hizo zote ndio maana amejitokeza. Pia alipohojiwa atatanuaje tatizo la rushwa iwapo ataingia madarakani, alisema ili kuondoa tatizo la rushwa jambo la kwanza ni kudhibiti vyanzo hivyo.
Alisema kutakuwepo na mikakati ili fedha zote zinazokusanywa zifike kwenye vyanzo husika na huduma zifike mahali panapostahili.

HABARILEO
Madereva wa mabasi watakaofanya mgomo bila kufuata utaratibu, wakati kukiwa na hatua za kutafuta ufumbuzi wa masuala yao watafukuzwa kazi, imeelezwa.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Nchini (TABOA), Enea Mrutu ambapo alisema, bado kuna mjadala unaoendelea hivyo si sahihi kwa madereva kugoma.
Alisema kama kuna dereva yeyote anayetaka kugoma, anapaswa mgomo huo akaufanyie kwa tajiri yake na si vituoni na kusababisha watu wengine kushindwa kuendelea na shughuli zao.
Mrutu alisema, hivi karibuni wakati Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta akiwasilisha bajeti yake, madereva hao waliitisha kikao bila kutoa taarifa kwa wamiliki, jambo lililosababisha wao kutoshiriki kikao hicho.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Nchini (Chamamata), Clement Masanja alisema mgomo wao utakuwa palepale endapo kikao cha serikali na wamiliki hakitatoa majibu ya matatizo yao.
Mambo hayo ni pamoja na utaratibu wa nauli ya kwenda na kurudi majumbani baada ya kazi, matibabu, usafiri, likizo pamoja na bima.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alisema, hawezi kuingilia mgogoro huo lakini kama watakwenda kumuona kama madereva walivyoahidi ataangalia namna ya kuwashauri.

JamboLEO
Muswada wa Haki ya Kupata Habari uliokuwa usomwe, kwa mara ya pili Jumamosi wiki hii, uko kwenye hatihati baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kukubali uondolewe na kurudishwa kwa wadau kwa ajili ya kuujadili kabla ya kurudishwa tena bungeni na kusomwa.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema jana kuwa baada ya kikao na Kamati ya Bunge, wamekubaliana kuwa muswada huo uliokuwa usomwe kwa mara ya pili unatakiwa kupata baraka za wadau.
“Kamati ya Bunge ilituita, lakini tuliwaambia yetu. Muswada ni mbovu, haujashirikisha maoni ya wadau na mambo mengi hayaendani na lengo la muswada,” alisema Mukajanga.
“Tuliwaambia muswada unakuja kwa mara ya pili, lakini ni bomu, na tumeiomba Kamati ya Bunge kumwambia Spika kuwa, kwa sasa, hakuna muda wa kuujadili, tupate muda wa kuujadili zaidi, ufanyiwe kazi kikamilifu,” alisisitiza.

Hata hivyo, Mukajanga alisema kuwa Kamati itamshauri Spika kuwa kuna haja ya kuujadili pamoja na kutoa muda zaidi wa kuufanyia kazi na hakuna sababu ya kuukimbiza kupitishwa.
Kwa upande wake Deus Kibamba alisema muswada huo utabana uhuru wa upatikanaji wa habari na kwamba kuruhusu kupitishwa kwa muswada huo, kutaviweka vyombo vya habari na waandishi wa habari katika wakati mgumu kutokana na sheria na kilichomo kwenye muswada wenyewe.
Alipoulizwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah kuhusu makubaliano kati ya MCT na Kamati ya Bunge ya Jamii, alisema wanasubiri taarifa kwa kuwa lazima mwenyekiti wa kamati amweleze Spika sababu za kuurudisha kwa wadau ndipo atoe uamuzi. “Kamati haina mamlaka ya kurudisha muswada kwa wadau,”alisema Dk Kashililah.

Wakati MCT pamoja na wadau wa habari wakikutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, jijini Dar es Salaam kilifanyika kikao cha wamiliki wa vyombo vya habari ambao wameiomba Serikali kuuondoa bungeni muswada huo hadi hapo watakaposhirikishwa, kwani ukipitishwa kuwa sheria utawanyima wananchi haki ya kupata habari.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald Meng alisema muswada huo ukipitishwa kuwa sheria, utavinyima uhuru wa usambazaji habari vyombo vinavyomilikiwa na watu binafsi, kitendo ambacho ni kinyume na Katiba ya nchi.

Post a Comment

0 Comments

Youtube Channel Image
Hajiizo Subscribe To watch more
Subscribe