Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed
Shein akitoa Risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa Wananchi na
Waislamu wote nchini katika Risala hiyo amewataka Wananchi kuwa amani na
Utulivu na kuwaombea kwa Mola wetu kuwajaalia Rehma baraka za Mwezi
Mtukufu wa Ramadhan pia amewataka kufanya ibada kwa wingi katika
kipindi chote cha mwezi huu,[Picha na Ikulu.]
Wassalamu Aleikum Warahmatullahi
Wabarakatu
RISALA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN YA RAIS WA
ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN,
MWAKA 1426 HIJRIYA, 2015 MILADIYA
BISMILLAHI RAHMANI RAHIM
Ndugu
Wananchi,
Assalamu Aleikum Warahmatullahi
Wabarakatu
Kwa wingi wa heshima
na unyenyekevu naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu; Subhana Wataala kwa kutupa
rehema na fadhila za kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mara nyengine
tena, tukiwa na amani, utulivu na salama nchini. RAMADHAN KARIM.
Mwenyezi
Mungu
ametujaaliya mwezi wa Ramadhani kuwa ni mwezi bora kuliko miezi
mengine. Huu ni mwezi ambao Yeye Mola wetu ameujaza sifa na sharia
Zake kwa
aya tano za Surat Al – Baqara, kuanzia
Aya ya 183 hadi Aya ya 187. Katika Aya 185 ya Sura hii, Mwenyezi Mungu
ameusifu
mwezi wa Ramadhani kwa kusema:
“Mwezi
wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Kurani ili iwe uongozi kwa
watu, na hoja zilizo wazi na uongozi wa upambanuzi (wa baina ya haki na
batili).”
Huo ni moja ya Utukufu wa
Mwezi wa Ramadhani ambapo Ibada za waja huwa na fadhila kubwa mbele ya Mwenyezi
Mungu. Kwa hivyo, tuna wajibu wa kujiandaa na kuweka azma ya kuzidisha Ibada
kwa wingi ikiwa ni pamoja na kufanya mambo yote ya kheri, kusali sala za
faradhi na sunna na kujifunza na kusoma sana Kurani. Tukumbuke kuwa huu ni
mwezi iliyoteremshwa Kurani. Kwa hivyo, kusoma Kurani na kuzingatia mafunzo
yake kuna fadhila kubwa. Kadhalika, Aya
tulioitaja inatubainishia kuwa Kurani ni uongozi ulio wazi, wa kubaini mambo
mabaya tukayaacha na mambo mema tukayaendeleza, ili tuweze kufanikiwa hapa
Duniani na kesho Akhera.
Ndugu
Wananchi,
Ramadhani ni mwezi
wa rehema na tunahitajiwa tuzidishe vitendo vya kufanya wema kwa wenzetu,
katika biashara na mambo mengine. Aidha, Kurani inatufundisha maadili mema ikiwemo
kuwa na moyo wa huruma na kuwasamehe wengine, hasa katika Mwezi huu Mtukufu wa
Ramadhani. Pamoja na mambo hayo tunahimizwa kutoa sadaka na kufunga. Kwa
kufanya hivyo, tutakuwa waumini wa kweli na wenye kutekeleza mafundisho ya
Kurani kama ilivyoelezwa katika Aya ya 92 ya Surat Al – Imran.
“Hamtaweza
kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda (nguo, vyakula, pesa) na
chochote mnachokitoa, basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua”. Tukumbuke kila
tunapotoa, Mola wetu atalipa kheri na hayo yameelezwa sana katika Qurani na
Hadithi za Bwana Mtume (S.A.W).
Kadhalika, Mola wetu
(SW) ametuambia katika Surat Sab’a, Aya 39 (Juzuu ya 22), yenye tafsiri
isemayo:
“Na
chochote mtakachotoa basi Yeye Atakilipa; naye ni Mbora wa wanaoruzuku”.
Kwa hivyo, huu ni wakati
wa kuwafikiria wengine, hasa wale wenye mahitaji katika kutekeleza saumu zao
ili nao waone rehema za Ramadhani. Hili
si jambo linalowahusu matajiri au wenye vyeo peke yao. Hazrat Abu Zarri amesema:
“Mtume
wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema, usifikirie kuwa kila kitendo kidogo kabisa
cha wema ni kuwa kidogo”.
Kila anayetoa basi
ajue malipo yake ni makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni vyema kutoa kwa
kuwapa wanaohitaji hasa kwa jamaa, majirani, marafiki na kadhalika.
Ndugu
Wananchi,
Katika mazingatio ya
kufanya wema (ihsani), na kufuata maadili, yanayotukuzwa katika mwezi huu
mtukufu wa Ramadhani, tunapaswa tuzingatie umuhimu wa kudumisha na kukuza amani
na utulivu. Ibada ya saumu inahitaji kuwepo kwa utulivu wa nafsi ili kuwapa
watu wasaa wa kuitekeleza Ibada hii yenye malipo makubwa kwa Mwenyezi Mungu.
Katika kuifikia hali hii, sote tuna wajibu wa kusimamia amani na utulivu ili
utekelezaji wa ibada zetu usiathirike.
Katika kufunga yapo mambo ya kuharibu funga (saumu) ya mfungaji.
Miongoni mwa mambo hayo ni kusema uongo na kuwafitini watu. Kwa hivyo, tujiepushe na mambo ya aina hiyo.
Lakini, badala yake, tuzidishe mapenzi baina yetu, tuhurumiane na tusaidiane
katika mambo yote ya kheri. Tuendeleze utamaduni wetu wa kula pamoja,
kufutarishana na kupelekeana vyakula vya tunu. Mambo haya yana umuhimu katika
kuendeleza mila na tamaduni njema za Wazanzibari. Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe
uwezo wa kuyafanya hayo.
Wakati huo huo,
nawanasihi wenye kumiliki mikahawa washirikiane na waumini wanaoutukuza Mwezi
huu Mtukufu katika kuondoa kero ambazo zinaweza kuwasababishia karaha
wanapoitekeleza ibada ya funga. Tudumishe utamaduni wetu wa kuheshimu dini.
Jambo ambalo limechangia kudumu kwa amani ya nchi yetu tangu kale na dahari.
Kila mmoja anapaswa kuhakikisha kuwa Mwezi wa Ramadhani unaheshimiwa kwa
vitendo. Kadhalika, wazazi nao
wanapaswa wawe waangalifu kwa watoto wao nyakati za usiku, ili wawe na nyendo
njema pamoja na kuwashajihisha kufanya ibada na kuhudhuria darsa
misikitini.
Vile vile, vyombo
vyetu vya ulinzi havina budi viimarishe doria za ulinzi katika maeneo yetu
mbali mbali, hasa kwa wakati ambao watu wengine wanakuwa katika shughuli za
Ibada. Zaidi ya hao, nawakumbusha madereva wazingatie sheria za usalama wa
barabarani kwa kutoendesha gari na vyombo vyengine kwa mwendo wa kasi; kwa
kisingizio cha kutaka watu wawahi kufutari na kupakia abiria zaidi, jambo
ambalo huhatarisha usalama wao. Askari wa usalama barabarani na taasisi
nyengine zinazohusika zina wajibu wa kulisimamia suala hili ipasavyo.
Ndugu
Wananchi,
Kama tunavyofahamu,
kwamba mahitaji huwa ni mengi zaidi
katika mwezi wa RamadhanI. Kwa baraka za
Mwenyezi Mungu, tulijaaliwa kupata mvua ambazo wakulima walizitumia vyema na tumeweza
kupata mazao mbali mbali ya chakula yakiwemo yale ambayo huwa yanatumika kwa
wingi katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Sambamba na hilo, Serikali
imeendelea kushirikiana na wafanyabiashara wetu katika utekelezaji wa sera ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutoa unafuu wa kodi katika uingizaji
nchini wa bidhaa muhimu za chakula ikiwemo mchele, unga wa ngano, sukari na
tende. Lengo la uamuzi huu wa Serikali
ni kuhakikisha kuwa chakula cha kutosha kinakuwepo katika kipindi chote cha
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kinapatikana kwa bei nafuu.
Ndugu
Wananchi,
Kama nilivyoeleza
katika miaka iliyopita, napenda nitumie fursa hii tena kwa mwaka huu
niwakumbushe wafanyabiashara wote kuwa msipandishe bei za bidhaa zenu bila ya
sababu za msingi. Wafanyabiashara wasivutiwe na kutaka kupata faida kubwa, bali
wawafikirie zaidi wananchi wenzao. Si jambo la busara kuutumia mwezi huu kwa
kuwapandishia bei wananchi, hasa wanyonge. Hatua hiyo ni kinyume na malengo ya
Serikali ya kupunguza unafuu wa kodi kwa bidhaa za chakula. Kwa bahati mbaya
wapo baadhi ya wakulima wenye tamaa ambao huamua kuleta sokoni mazao ambayo
hayajapea. Wakulima hawa si waadilifu kwa hivyo, taasisi zinazohusika zina
wajibu wa kusimamia taratibu na
utekelezaji wa Sheria ya kumlinda mtumiaji, ikiwa ni pamoja na kuwaepusha
kuuziwa bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umemalizika.
Ni dhahiri kuwa
katika Mwezi wa Ramadhani shughuli za biashara huimarika zaidi. Nawanasihi
wafanyabiashara kuendelea kuzingatia sheria. Biashara zote zifanywe katika
maeneo yaliyoruhusiwa ili kuepusha usumbufu na msongamano usio wa lazima.
Kadhalika, wafanyabiashara pamoja na wafanyakazi wa Baraza la Manispaa kwa mji
wa Unguja na Mabaraza ya Miji ya Pemba, waongeze juhudi zao katika kuimarisha
usafi wa miji yetu. Uzoefu unaonesha kuwa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani taka huwa zinaongezeka. Kwa hivyo, jitihada zaidi zinahitajika katika
kuimarisha usafi wa miji yetu. Tukumbuke kwamba Uislamu unahimiza sana
unadhifu.
Kama nilivyoiagiza
Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA) katika Ramadhani za miaka iliyopita na mwaka
huu naiagiza tena ZAWA na Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kufanya kila jitihada ili iwapatie maji
wananchi kwa kutumia magari katika sehemu zote ambazo huduma za maji safi na
salama zina upungufu. Natoa wito kwa wananchi washirikiane na Mamlaka hiyo, ili
kuifanikisha shughuli hiyo ipasavyo.
Ndugu
Wananchi,
Wakati tunapokuwa
katika Mwezi Mtukufu, ni vyema tukawa tunazingatia matayarisho ya ibada ya Hija
kwa wale wanaokusudia kwenda Hija mwaka huu.
Muda uliobaki ni mfupi na kutokana na sheria za sasa za Hija,
matayarisho yanalazimika kukamilishwa mapema zaidi mwaka huu. Namuomba Mwenyezi Mungu awape baraka wale
wote wanaojiandaa na watakaojaaliwa kwenda kuhiji mwaka huu na awajaalie kheri
na safari ya salama.
Ndugu
Wananchi,
Napenda nimalizie
risala yangu kwa kukutakieni nyote kheri, rehema na Baraka za Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani. Namuomba Mola wetu atupe nguvu na uwezo wa kuendeleza ibada za saumu,
na ibada nyengine katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na kudumisha na
kuendeleza amani, umoja na mshikamano. Tumuombe Mwenyezi Mungu atujalie
Ramadhani njema.
Ahsanteni,
RAMADHAN KARIM
0 Comments