Wanasiasa wananchi mashuhuri nchini walioko katika kambi zenye upinzani mkubwa wa kisiasa watakutana jumatano Mkoani Kilimanjaro.
Wanasiasa hao ambao ni Rais Kikwete, mgombea Urais Dk. MAGUFULI, LOWASSA pamoja na Freeman Mbowe wanatarajia kukutana katika mazishi ya muasisi wa TANU na CCM marehemy Peter Kisumo.
Lowassa ni mgombea Urais Chadema ambaye atapeperusha bendera kupitia umoja wa katiba ya wananchi UKAWA akishindana na Magufuli aliyeteuliwa na vikao vya juu vya CCM kuwa mgombea wake wa Urais licha kuwepo manung’uniko kuwa uteuzi wake haukufuata utaratibu.
Taarifa zinasema wanasiasa hao watahudhuria mazishi hayo yaliyopangwa kufanyika Augusti 13 Mkoani Kilimanjaro.
Rais Kikwete ndiye anayetarajiwa kuwaongoza wakazi wa Kilimanjaro katika mazishi hayo ya aliyekuwa mwasisi wa TANU na baadaye CCM.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amesema sasa atazungumza lugha moja na wakwe zake baada ya kukamilika Barabara ya Ndundu-Somanga kwa kiwango cha lami.
Rais Kikwete alisema hayo juzi jioni kwenye sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo iliyofanyika Kijiji cha Marendego Mpakani na kuhudhuriwa na wananchi wa mikoa ya Lindi, Pwani pamoja na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali akiwamo Balozi wa Kuwait nchini, Jassem Ibrahim AL- Najem.
“Nimekuwa mwenye furaha sana maana barabara hii ilikuwa ikininyima usingizi kwa sababu mbili; kwanza kuchelewa kumalizika na vilevile kile kilio cha kuhitaji hii barabara ilikua ni kilio cha muda mrefu sana cha wananchi wa mikoa hii ya kusini cha wabunge wao na viongozi wao.
“Lakini siyo hilo pekee, kwa sisi tuliooa mikoa ya huku, imenipa tabu pia, kila wakati naulizwa mbona humalizi barabara ya kwetu, ninasema itaisha, kwa hiyo nafurahi leo ndugu Magufuli (John) umeniondolea unyonge, ninasimama hapa kwa kujiamini. Wakwe zangu na shemeji zangu ugomvi sasa umeisha, kwa hiyo nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitakushukuru Waziri Magufuli. kwa kuwa mstari mbele kusimamia ujenzi huu na hata katika maeneo mengine umekuwa mtendaji wa kuigwa,” Kikwete
Akitoa taarifa ya barabara hiyo Dk Magufuli alisema sehemu hiyo ya kilomita 60 ndiyo iliyokua sehemu pekee iliyobaki kujengwa kwa kiwango cha lami, mradi huo umegharimu Sh77.2bil na kutekelezwa kwa kugharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 55, Mfuko wa Kuwait kwa asilimia 31 na mfuko wa OPEC kwa asilimia 14.
Naye Balozi AL-Najem alisema kwamba ziara ya Rais Kiwete nchini humo ndiyo chimbuko ya mafanikio ya barabara hiyo.
Mapema mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo akitoa salamu za mkoa alisema awali usafiri wa wananchi kutoka Ndundu ilichukua siku mbili hadi tatu kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara au kutoka kwenye mikoa hiyo kuja Pwani na Dar esaaam kutokana na eneo hilo kuwa mbaya na hivyo magari mengi yalikuwa yanakwama kuendelea na safari yakifika hapo lakini sasa safari ni kwa saa,” alisema.
MWANANCHI
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye alianguka katika hatua za awali za mbio za urais ndani ya CCM, amesema ameishia kuwa “rais wa fikra”.
Pinda, ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa takriban miaka minane, hakuweza kuingia katika orodha ya makada watano ambao majina yao yalipelekwa Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupata majina matatu ya kupelekwa Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Baada ya mchakato huo kumalizika, mbunge huyo wa Katavi amekuwa kimya, lakini jana aliibuka na kuzungumzia mbio hizo zilizoacha majeraha kwenye chama hicho kikongwe.
Pinda alisema mchakato huo ulikuwa hauna kulala, wa haraka haraka, ambao uliisha kwa CCM kupata mgombea ambaye alimuelezea kuwa “ni chaguo la Mungu”.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa fupi ya Mkoa wa Mbeya kuhitimisha maonyesho ya Nanenane jijini hapa, Pinda alisema alitamani sana kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.
“Mimi ninaamini Mungu ndiye anayepanga kwani sikuzaliwa kuwa Waziri Mkuu wala kuwa Rais, lakini nilipangiwa uwaziri mkuu ambao nimefanya kazi hiyo hadi nimechoka,” alisema Pinda, ambaye alikuwa mmoja wa makada 42 wa CCM waliojitokeza kuwania ridhaa ya chama hicho kugombea urais.
“Baada ya mchakato ule, alipatikana mtu mahiri ambaye Mungu alimpanga, lakini tamaa yangu, ikaishia kuwa rais wa fikra tu.”
Alisema mchakato ulifanyika kwa kasi bila kulala na wakapatikana watano, mara watatu na hatimaye mmoja.
“Suala hilo halitakiwi kuwa sababu ya kugombana, kulaumiana na kutoana macho, kwani ni sawa na kugombana na Mungu,” alisema Pinda.
“Hata mimi nilitamani sana kuwa Rais, lakini sasa yamekwisha. Sina sababu ya kuwa na hasira au kuhama chama kwani haina tija na hasira ni hasara.
“Sina sababu ya kuhama chama, nitabaki CCM na baada ya Oktoba nitakuwa mkulima mzuri ambaye nitashirikiana na wenzangu kuendeleza nchi.” Pinda alisema mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ni mzuri na kwamba Mungu atamsaidia kujua mahitaji mengine ya Taifa na Watanzania.
Alisema ana uhakika kwamba ifikapo mwaka 2025, hali ya umaskini katika kaya itakuwa imepungua.
Aliwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na maofisa wote wa Serikali waliogombea urais, ubunge na udiwani ambao walishindwa katika kura mbalimbali, wakubali matokeo na wachape kazi bila kinyongo na kwamba Serikali ijayo itawafikiria kwa utendaji mzuri.
MWANANCHI
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kesho atachukua fomu za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati msafara wake utakapoanzia ofisi za makao makuu ya CUF kuelekea ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na baadaye kwenda kumalizia makao makuu ya Chadema yaliyoko Kinondoni.
Safari ya Lowassa, ambaye anawania urais kwa tiketi ya Chadema na chini ya mwamvuli wa vyama vinne vya CUF, NCCR-Mageuzi, Chadema na NLD, itakuwa ya umbali wa kilomita 11, ikihusisha wilaya mbili za Ilala na Kinondoni.
“Yeyote anayejisikia kutaka kumsindikiza Lowassa, anakaribishwa,” alisema kaimu katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu jana alipozungumza na waandishi wa habari.
“Tutaanzia CUF na kumalizia Chadema. (Lowassa) ataambatana na mgombea mwenza, Juma Duni Haji.”
Kwa mujibu wa Mwalimu, msafara huo utaanzia ofisi hizo za CUF zilizoko Buguruni na kwenda katikati ya jiji, takriban kilomita tano, ambako Lowassa atachukua fomu ofisi hizo za NEC na baada ya tukio hilo, msafara utakwenda Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, takriban kilomita sita, ambako ni makao makuu ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Lowassa, ambaye alibadili upepo wa mbio za urais baada ya kuihama CCM na kujiunga na Chadema iliyompa fursa ya kuwania nafasi hiyo, atakuwa mtu wa saba kuchukua fomu hizo tayari kwa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Wengine waliochukua fomu hizo ni John Magufuli wa CCM, Mchungaji Christopher Mtikila (DP), Chifu Lutayosa Chemba (ADC), Macmillan Limo (TLP), Hashimu Rungwe (Chauma), Fahami Dovutwa (UPDP) na Dk Godfrey Malisa (CCK).
Akiongea na waandishi wa habari makao makuu ya NCCR jana, Mwalimu alisema msafara wa kumsindikiza Lowassa utaanzia saa 3:00 asubuhi.
Alisema mara baada ya kukamilisha kazi ya uchukuaji fomu, kuanzia Agosti 14, Lowassa ataanza ziara katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutafuta wadhamini, ikiwa ni baada ya kushiriki mazishi ya kada mkongwe wa CCM, Peter Kisumo yatakayofanyika Agosti 13, mkoani Kilimanjaro.
“Hatakwenda mikoa yote kutokana na muda, lakini tatizo jingine kila mwanachama anataka mgombea wetu (Lowassa) aende mkoa aliopo. Hili limetupa tabu na ndiyo sababu ya kubadilika kwa ratiba zetu,” alisema.
“Tutaeleza ratiba kamili na katika mikoa ambayo Lowassa hatafika kwa sasa, atafika wakati wa kampeni,” alisema Mwalimu.
Kuhusu ugawaji wa majimbo, Mwalimu alisema kazi hiyo imeshafanyika na siku yoyote kuanzia leo watatangaza.
“Tumeyagawa majimbo yote yakiwemo yale 26 mapya kwa kuzingatia umoja wetu wa Ukawa. Najua siku zimebaki chache kabla ya uchaguzi mkuu, hivyo tutatangaza tu kuanzia kesho (leo),” alisema.
MWANANCHI
CCM imesema haitarudia makosa ya mwaka 2010 ya kutengua uamuzi wa wanachama, lakini itahitaji kuwa na moyo mgumu baada ya makada wengi kukata rufaa kupinga matokeo ya kura za maoni.
CCM inamalizia hatua ya mwisho ya mchakato wake wa ndani wa kupata wagombea ubunge na udiwani kwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vitakavyopitia majina ya makada wote walioshinda kwenye kura za maoni, ambazo zilitawaliwa na tuhuma za rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Vikao hivyo huwa vinaweza kutengua ushindi wa kada kwenye kura za maoni kwa kuangalia rufani zinazopinga mchakato, tuhuma za rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema wamepokea malalamiko mengi kuhusu ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi katika upigaji wa kura za maoni.
“Kumekuwa na utamaduni wa kulalamika barabarani wakati mwingine kushawishi wanachama kulalamika kwenye vyombo vya habari na kwingineko. Utaratibu huu si wa chama chetu,”Nape.
“Tunashauri taratibu zifuatwe. Katika kufikia hatua hii tunawaomba wanachama wawe watulivu.”
Alisema wanachama wamejaa mjini Dodoma wakijaribu kushawishi wajumbe kuhusu rufaa zao, lakini akasema kinachotakiwa kiwasilishwe ni malalamiko yao, ushahidi wa kutosha katika ngazi husika.”
Nape pia alisema kumezuka wimbi la matapeli linalowalaghai makada walioshindwa katika kura za maoni kuwa watoe fedha ili wawasaidie rufaa zao kwenye vikao hivyo.
Alisema matapeli hao wamesajili namba za simu za viongozi wa CCM na kwamba yeye ni mmoja wa viongozi walioathirika na utapeli huo kwa namba yake ya simu ya mkononi kutumika.
MWANANCHI
Mjumbe wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole amesema yupo tayari kufanya kampeni za kumpinga mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa kwa madai kuwa ana doa linalomzuia kuwania nafasi hiyo.
Polepole ameibuka kuwa maarufu tangu kumalizika kwa Bunge la Katiba, akishiriki kwenye midahalo kadhaa kuhusu mchakato wa kuandika Katiba mpya, akitofautiana na msimamo wa CCM wa kubadilisha Rasimu ya Katiba.
Akizungumza na Mwananchi jana, Polepole alisema Lowassa anayeungwa mkono na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ana tuhuma za ufisadi na ni mmoja wa makada wa CCM walioipinga Rasimu ya Katiba.
Polepole alisema msingi wa kuzaliwa kwa Ukawa ni kutaka Katiba mpya yenye maoni ya wananchi, hivyo Chadema kumpokea Lowassa ni sawa na kukiuka misingi hiyo.
“Nimeshirikiana na Ukawa na viongozi wao kama Watanzania kuhakikisha Taifa letu linapata Katiba mpya na inayotokana na maoni ya wananchi. CCM ambao walikuwa ndiyo wana mkakati na wenye maamuzi ya mwisho katika kukwamisha maoni ya wananchi. Watu hao (wa CCM) hawastahili kupewa uongozi iwe ndani ya CCM au hata ndani ya Ukawa,” alisema.
“Hawana dhamira njema na Taifa letu, watuhumiwa mengine nitaelewa, lakini kwenye la Katiba nilikuwepo na ninajua mchango wao wa kutukwamisha. Niliweka maoni yangu kwamba CCM ikiwachagua hao nitapiga kampeni ya kuwakataa. Hawakupita CCM na mmoja wapo ni Lowassa.”
Alisema amepoteza imani na Ukawa kwa kukubali kuikiuka misingi ambayo awali waliisimamia.
“Nina haki ya kutokubaliana na msimamo wa Ukawa na ikibidi nitasimama na kupiga kampeni ya kumkataa mgombea wao wa urais,” alisema.
Katika Bunge la Katiba, wajumbe kutoka CCM walilazimisha kuondolewa kwa baadhi ya mapendekezo kwenye Rasimu ya Katiba, ikiwa ni pamoja na pendekezo la kutaka muundo wa Muungano uwe wa serikali tatu.
SOURCE: millardayo.com
0 Comments