Kura
za maoni za kuwapata wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa ubunge na
uwakilishi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu zimetawaliwa
na vitendo vya rushwa.
Kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (Zaeca),
imewakamata makada kadhaa wa chama hicho, wakituhumiwa kugawa rushwa ya
fedha, nguo na wengine kuunganishwa umeme kwenye nyumba zao.
Akizungumza katika mahojiano maalum na
NIPASHE, Mkurugenzi wa Zaeca, Mussa Haji Ali, alisema makada wengi
wakiwamo vigogo wa chama hicho wanatuhumiwa kutoa rushwa katika mchakato
huo.
Alisema
maofisa wake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waliwakuta wanasiasa
hao kwenye maeneo mbalimbali wakitoa rushwa kwa wana-CCM na viongozi wa
matawi wa chama hicho.
Alisema kuwa miongoni mwa vitu walivyokutwa wakigawa wakiwa kwenye kampeni ni fedha taslimu, kanga na kofia.
Alisema
uchunguzi dhidi ya makada hao ukikamilika, watawasilisha majalada ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa ajili ya kufungua mashitaka.
Alisema wanao ushahidi wa kunaswa na vipaza sauti, wa picha za mnato na picha za video .
Mmoja wa watuhumiwa ni aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Magomeni.
Alisema
mgombea huyo alitiwa nguvuni nyumbani kwake wakati akiwagawia kofia
watu 40, doti za kanga na fedha taslimu kwa makatibu wa matawi wa chama
hicho.
Mkurugenzi
huyo wa Zaeca, alisema wamewakamata watu waliojitambulisha kuwa ni
wapambe wa aliyekuwa miongoni mwa wagombea wa Jimbo la Paje kwa nafasi
ya uwakilishi na ubunge kati ya hao akiwa na Sh. 850,000 na doti 100 za
kanga.
Taasisi hiyo pia ilimkamata mgombea ubunge mmoja wa jimbo la Chwaka, akigawa Sh. 5,000 kwa kila mwanachama.
Alisema
katika maeneo ya Kibirikani Fuoni alikutwa mgombea uwakilishi akigawa
fedha, lakini baada ya kupata taarifa kuwa Zaeca wameizunguka nyumba
hiyo, alichoma moto gari aina ya PRADO na kukimbia.
Wengine
ni mgombea ubunge wa Jimbo la Magomeni, ambaye alitoa fedha katika
akaunti yake na kumtumia mtu kuwagawia wapiga kura huku mgombea mwengine
wa jimbo hilo kwa nafasi hiyo hiyo akidaiwa kutoa fedha Benki ya CRDB
na kuwatumia wanachama kupitia simu.
Katika jimbo la Amani, mamlaka hiyo ilimkamata mgombea uwakilishi akigawa mchele.
Mamlaka
hiyo pia imemnasa mgombea wa ubunge Jimbo la Mpendae, akigawa jezi na
mipira kwa timu mbili za soka na Sh. 250,000 huku akikusanya mabalozi wa
zoni tatu na kuwapa Sh. 5,000. Anadaiwa kuwagawia viongozi wa matawi
Sh. 10,000 kila mmoja.
Pia anadaiwa kuwakusanya watu wasiopungua 40 katika Chuo cha Msolopa Kilimani na kuwapa Sh. 5,000 kila mmoja.
Katika
Jimbo la Malindi, Zaeca ilimkamata mgombea ubunge akigawa Sh. 5,000 na
watu watatu ambao baada ya kuhojiwa walikiri kuzipokea.
Alisema
katika Jimbo la Kikwajuni walimnasa mgombea ubunge katika eneo la
Michezani na Sh. milioni 10 akiwa amewakusanya makatibu wa CCM jimbo na
wasimamizi wa uchaguzi ili kuwagawia fedha hizo.
Kwa
mujibu wa Ali, mgombea uwakilishi mmoja alikutwa akivikusanya vikundi
vya kinamama kwa kutoa Sh. 5,000 kwa kila mmoja katika maeneo ya Muembe
Ladu.
Yumo
pia mmoja wa wagombea ubunge wa Jimbo la Chumbuni aliyekutwa
akivikusanya vikundi 10 katika tawi la CCM na kukipatia kila kimoja Sh.
150,000.
Ali
aliongeza kuwa mmoja wagombea uwakilishi jimbo la Mfenesini, alikutwa
akiwa na mkewe maeneo ya Mwakaje wakitoa fedha na kwamba baada ya
kuwaona watendaji wa Zaeca, mkewe alikimbia huku dereva akikutwa na Sh.
500,000.
Katika
jimbo la Tumbatu, mgombea wa ubunge alikamatwa akidaiwa kusambaza nguzo
za umeme na kuwaunganishia umeme wakazi wa kijiji cha Tumbatu kwa
gharama zake.
Katika Jimbo la Donge mmoja wa wagombea ubunge alitumia wapambe wake kuwapa wapiga kura fedha.
Kwa
upande wa viti maalum vya ubunge na uwakilishi, taasi hiyo pia iliwatia
mbaroni wagombea watatu wa ubunge na watatu wa uwakilishi wanaodaiwa
kuwakusanya wakazi 30 wa maeneo ya Pangawe na Kijitoupele na kuwapa Sh.
100,000 kila mmoja. >>> stori zaidi ziko hapa
http://www.zanzinews.com
http://www.zanzinews.com
CHANZO: NIPASHE
0 Comments