Habari

6/recent/ticker-posts

Header Ads Widget

Advertise with us here

HPV: Ugonjwa wa zinaa unaoweza kusababisha Saratani ya shingo ya kizazi

Human Papillomavirus 
HPV ni moja ya magonjwa yanayoenezwa kwa njia ya ngono, wanaume na wanawake wako katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu. HPV ni kifupi cha neno Human Papilloma Virus, kundi la virusi lenye aina zaidi ya 150 ya virusi vinavyohusiana.

HPV ni kirusi kinachoweza kuambukiza kutoka mtu mwenye maambukizi hadi kwa asiye na maambukizi kwa njia ya kugusana ngozi wakati wa tendo la ndoa. Virusi hivi huvutiwa na ngozi na sehemu zenye unyevunyevu kama kwenye uke, njia ya haja kubwa, kichwa cha uume, mdomo, koo na mapafu. Virusi hivi hushindwa kusitawi kwenye sehemu zingine za mwili pia.
Virusi vya HPV vipo dunia nzima ingawa maambukizi mengi ya HPV hayasababishi dalili, maambukizi ya HPV sehemu za siri yakiendelea kwa muda mrefu husababisha saratani ya shingo ya kizazi. 

Virusi vya HPV vinaweza pia kusababisha aina zingine za saratani katikati ya makalio, saratani ya kichwa na shingo na chunjua za sehemu za siri (Genital Warts) yaani sugu katika sehemu za siri kwa jinsia zote.

Aina za 6 na 11 za  virusi vya HPV husababisha sugu sehemu za siri (genital warts) wakati saratani mbalimbali husababishwa na aina za 16, 18, 31, 33, 45, 52 na 58 za virusi vya HPV.
Mamilioni ya watu ulimwenguni pote huambukizwa virusi hivyo ambavyo inasemekana ndio ugonjwa wa zinaa ambao huwapata watu wengi zaidi. Pia, virusi hivyo ndivyo kisababishi kikuu cha saratani inayowaua wanawake wengi katika nchi maskini.
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), virusi hivyo ndivyo kisababishi kikuu cha saratani ya shingo ya kizazi  ambayo inashikiria nafasi ya pili katika saratani zote zinazowaathiri wanawake duniani kote.

Kila mwaka, mamia ya maelfu ya wanawake huchunguzwa na kupatikana na virusi vya HPV na kila mwaka maelfu hufa kwa sababu ya saratani ya shingo ya kizazi ambayo husababishwa na virusi hivyo.

Mwaka 2008, kulikuwa na kadirio la kesi mpya 529, 000 za saratani ya shingo ya kizazi huku kukiwa na vifo 274, 000 kutokana na saratani hiyo. Zaidi ya 85% ya vifo vinatokana na saratani ya shingo ya kizazi hutokea nchi zinazoendelea, ambayo ni 13% ya saratani zote za wanawake.

Virusi vya HPV hufanya wanaume na wanawake wapatwe na vipele vigumu, kutia ndani vipele vinavyotokea kwenye viungo vya uzazi. Kwa kawaida, vipele hivyo havina kansa. Ingawa kuna aina za virusi vya HPV zaidi ya 150, ni chache sana kati yazo ambazo husababisha kansa.
Mtu hupata saratani ya shingo ya kizazi ikiwa tu aina fulani ya virusi hivyo vinakaa kwa muda mrefu. Kwa upande mwingine, maambukizo mengi ya virusi hivyo hupona yenyewe baada ya kushindwa nguvu na mfumo wa kinga wa mwili.

Ni kina nani wanaweza kuambukizwa?
 
Wale hasa wanaoweza kuambukizwa ni wanawake wanaoanza kufanya ngono wakiwa na umri mdogo, wale walio na wapenzi wengi wanaume, au wale wanaofanya ngono na mwanaume ambaye ana wapenzi wengi wanawake. Mara nyingi, mwanamume asiye na dalili zozote zinazoonekana za ugonjwa huo ndiye humwambukiza mwenzi wake.

Hata hivyo, katika visa fulani, wanawake walio safi kiadili au wale ambao labda hawajawahi kufanya ngono huambukizwa virusi hivyo. Kwa mfano, uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba mtoto anaweza kuambukizwa virusi hivyo mama anapojifungua, au mtu anaweza kuambukizwa kwa njia nyingine. Ugonjwa huo unaweza kujitokeza miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa.
Pia, kuna mambo kadhaa yanayofanya mtu awe katika hatari kubwa ya kupata HPV, mfano kuwa na upungufu wa kinga mwilini kama wenye VVU, kuwa na mikwaruzo/vidonda kwenye ngozi hasa sehemu za siri, kugusana na mtu mwenye chunjua (warts). Jambo jingine ni umri ambapo chunjua za kawaida hutokea kwa watoto, chunjua za sehemu za siri (Genital Warts) hutokea kwa waliobalehe na watu wazima na chunjua za visigino (Plantar Warts) hutokea kwa watu wazima ingawa huanza kwa vijana.

Jinsi ya kujua endapo umeambukizwa
 
Dalili za ugonjwa huo hazijitokezi waziwazi. Ikiwa chunjua (warts) zinaonekana, mtaalamu wa afya anaweza kutoa bainisho (diagnosis) la ugonjwa huu baada ya kutazama kwa makini. Vipimo vya ziada vinaweza kufanyika ili kutathmini kwa undani uwepo wa HPV.  Hatua muhimu ni kufanyiwa uchunguzi wa chembe za mlango wa tumbo la uzazi, yaani pap smear, au Papanicolaou Smear.
Ikumbukwe kuwa, uchunguzi huo ulipewa jina la daktari Mgiriki, George N. Papanicolaou, ambaye alivumbua mbinu ya kutia chembe rangi ili kuzichunguza.

Ili kufanya uchunguzi huo, daktari hutoa chembe chache za mlango wa tumbo la uzazi na kuzipeleka kwenye maabara ili zichunguzwe. Uchunguzi huo unaweza kuonyesha ikiwa mtu ameambukizwa, ana uvimbe, au ana chembe zisizo za kawaida. Inaripotiwa kwamba uchunguzi wa pap smear umepunguza idadi ya watu wanaopatwa na saratani ya shingo ya kizazi na vifo vinavyosababishwa na kansa hiyo.

Ikiwa matokeo ya uchunguzi huo hayaridhishi, kifaa maalumu chenye kamera hutumiwa kuchunguza sehemu iliyoathiriwa. Kwa kutumia kifaa hicho, daktari anaweza kuona ikiwa kuna kidonda. Sehemu za tishu zilizoathiriwa hukatwa na kufanyiwa uchunguzi, kisha matibabu huanza. Siku hizi, uchunguzi wa hali ya juu sana, unaweza kufanywa kwenye maabara. Uchunguzi huo unaweza kuonyesha vizuri zaidi ikiwa mtu ameambukizwa.

Nini matibabu na kinga?
 
Mara chache chunjua huisha zenyewe bila matibabu ingawa kuna matibabu kadhaa yanayoweza kudhibiti maambukizo ya HPV. Wataalamu hutumia dawa za kupaka. Baadhi ya dawa hizo huharibu chembe zenye virusi hivyo, na wengine husaidia mfumo wa kinga kupambana na virusi hivyo. Matibabu mengine hutia ndani kuondoa sehemu iliyoathiriwa kwa kutumia umeme, leza, au kwa kuigandisha. Ni muhimu kuzungumza na daktari ili akusaidie kuchagua matibabu kulingana na aina ya chunjua zinazokukabili.

Chanjo kuu mbili za HPV zinazotafutiwa soko nchi nyingi duniani kote zina uwezo wa kuzuia maambukizi ya virusi vya aina ya 16 & 18 ambavyo kwa pamoja husababisha 70% ya kesi zote za saratani ya shingo ya kizazi duniani kote. Chanjo moja inaweza kuzuia chunjua za katikati ya makalio na sehemu za siri (anogenital warts) ambazo husababishwa na HPV aina ya 6 & 11. Kundi kubwa linalolengwa kwa ajili ya chanjo hizi ni wasichana waliobalehe duniani kote.
Walioambukizwa wanapaswa kujua ingawa chunjua (warts) zinaweza kuondolewa au kuondoka zenyewe, kirusi cha HPV kinaweza kubaki kwenye mwili wako na unaweza kuendelea kuwaambukiza wengine kwa maana hamna matibabu yatakayotoa kirusi cha HPV ndani ya mwili wako.

Mtu anawezaje kuepuka kuambukizwa?
 
Usifanye ngono kabla hujaolewa. Pia ili kuzuia saratani ya shingo ya kizazi, ni lazima wenzi wawe waaminifu. Hata hivyo, ni muhimu kujua kuhusu HPV kwa kuwa unaweza kuzuia usiambukizwe virusi hivyo. Isitoshe, hata kama maambukizo hayo yanajitokeza na kuenea, bado unaweza kutibiwa.
Shirika la WHO linasema: 'Mara nyimgi saratani ya shingo ya kizazi inaweza kutibiwa ikigunduliwa mapema.' Mbali na kujifunza kuhusu maadili, wanawake wanapaswa kujua kuhusu ugonjwa huo na kuelewa umuhimu wa kufanyiwa uchunguzi mbalimbali kwa ukawaida kama vile pap smear.

Uchunguzi huo unapaswa kufanyiwa mtu anapofikia umri wa miaka 18 au anapoanza kufanya ngono. Kasoro yoyote ikigunduliwa, mwanamke anaweza kutibiwa. Bado wanasayansi wanaendelea kutafuta njia rahisi na zenye matokeo zaidi za kuchunguza virusi vya HPV. Pia, chanjo za kuzuia na kutibu ugonjwa huo zinaendelea kutengenezwa.

SOURCE: Habari hii nimeipata kwenye website ya Fikra Pevu kutoka kwa 

Post a Comment

0 Comments

Youtube Channel Image
Hajiizo Subscribe To watch more
Subscribe